CHAMA CHA CM-TANZANIA CHAFUTIWA USAJILI.
Msajili
wa Vyama vya Siasa nchini amekifuta katika orodha ya vyama vya siasa
vyenye usajili wa muda Chama cha Maadili na Uwajibikaji(CM-Tanzania) kutokana na kushindwa kutimiza masharti ya usajili.
Chama cha CM-Tanzania kilipata usajili wa muda tarehe 4 Februari, 2016.
Kwa
mujibu wa kifungu cha 8(3) na (4) cha Sheria ya Vyama vya Siasa namba 5
ya mwaka 1992, chama cha siasa chenye usajili wa muda ni lazima
kiwasilishe maombi ya usajili wa kudumu ndani ya siku mia moja na
themanini tangu tarehe ya kupata usajili wa muda. Aidha, uhai wa chama
cha siasa chenye usajili wa muda unaisha baada ya siku mia moja na
themanini (180) tangu kipate usajili wa muda .
Hivyo,
uhai wa cheti cha usajili wa muda wa Chama cha Maadili na Uwajibikaji
(CM-Tanzania) ulikwisha tarehe 2 Agosti, 2016, kwani waanzilishi wake
walipaswa kuwasilisha maombi ya usajili wa kudumu siyo zaidi ya tarehe
02 Agosti, 2016.
Kwa
mujibu wa Sheria ya Vyama vya Siasa, waanzilishi na wanachama wote wa
CM-Tanzania hawapaswi kufanya siasa au shughuli yoyote kwa jina la Chama
cha Maadili na uwajibikaji, kwa sababu uhai wa cheti chake cha usajili
wa muda umekwisha. Kufanya hivyo ni kukiuka Sheria za nchi.
Kufutwa
kwa Chama cha Maadili na Uwajibikaji kunaifanya idadi ya vyama vya
siasa vyenye usajili wa muda kuwa kimoja ambacho ni Chama cha
Restoration of the Nation Party (RNP). Aidha, idadi ya vyama vya siasa
vyenye usajili wa kudumu ni ishirini na mbili (22).
Leave a Comment