SERIKALI imelifungia gazeti la MSETO ambalo ni Gazeti moja wapo yanayomilikiwa na Mbunge wa Ubungo,Saed Kubenea kwa kipindi cha
miaka mitatu kuanzia leo kwa kile ilichodai kuwa ni gazeti hilo kuchapisha
habari iliyoambatana na nyaraka ilizoziita za kughushi, anaandika
Regina Mkonde.
Nape Nnauye Waziri wa Habari, Utamaduni,
Sanaa na Michezo amedai kuwa uamuzi huo umefanywa na serikali ya awamu ya tano
kutokana na kutoridhishwa na mwenendo wa uandishi wa gazeti hilo.
Nape amewaambia wanahabari kuwa, “Serikali kwa
masikitiko makubwa imelazimika kuchukua uamuzi huu kutokana na mwenendo wa
uandishi wa gazeti hilo wa kuandika na kuchapisha habari ya uongo na kughushi
kwa kutumia nyaraka mbalimbali za serikali kwa nia ya kumchafua Rais na
viongozi wa serikali.”
Habari iliyoliponza gazeti hilo ni ile ya toleo Na.
480 la tarehe 4 hadi 10 Agosti 2016 ikiwa na nyaraka (barua) kutoka Shirika la
Madini la Taifa la (STAMICO) yenye kichwa cha habari; “Waziri Amchafua JPM”
Amhusisha na rushwa ya uchaguzi mkuu, ni Naibu Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano.
Barua hiyo inaonyesha kuwa Serikali kupitia kwa
Mhandisi Edwin Ngonyani Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano wakati
huo akiwa Kaimu Mkurugenzi mtendaji wa STAMICO iliandika barua ya kushukuru
kupokea fedha zaidi ya dola za kimarekani 65,000/= kwaajili kampeni kutoka kwa
mwekezaji James Sinclair.
Serikali imefanya maamuzi ya kulifungia gazeti la
MSETO kwa mujibu wa Sheria ya Magazeti ya mwaka 1976 sura ya 229 kifungu cha
25(1) ambayo imekuwa ikilalamikiwa na wanahabari kwa zaidi ya miongo mitano
sasa, sheria hiyo inatajwa kuwa ni kandamizi kwa vyombo vya habari.
Wanahabari wamekuwa wakipendekeza sheria hiyo
inayompa mamlaka Waziri anayeshughulikia masuala ya habari kukifungia chombo
chochote cha habari iwapo, kwa mtazamo wake binafsi ataona chombo hizo
hakizingatii maslahi ya umma. Hakuna ufafanuzi juu ya neon ‘maslahi ya umma’ na
kipimo chake.
Sheria hiyo inatamka katika kifungu cha 25(1);
“Waziri akiona kwamba kwa ajili ya maslahi ya umma au kwa ajili ya kudumisha
amani na usalama, aweza kutoa amri na kutangaza kwenye gazeti la serikali
ambayo itaeleza kwamba gazeti lililotajwa katika amri hiyo litasitisha kutolewa
tangu siku itakayotajwa katika amri hiyo.”
Aidha serikali pia imetangaza kusitisha uchapishwaji
wa gazeti la MSETO kuchapishwa katika njia nyingine zote za upashanaji habari
ikiwemo mitandao. Uamuzi huu umetangazwa kufanywa kwa kutumia Sheria ya
Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta sura ya 306.
Hili ni gazeti la pili kufungwa na Serikali ya awamu
ya tano katika kipindi cha miezi saba, ambapo Januari mwaka huu serikali
ilitangaza kulifutia usajili kabisa gazeti la MAWIO kwa madai ya kuandika
habari za uchochezi kwa muda mrefu.
No comments:
Post a Comment